Uongozi wa Ihefu FC umegonga hodi Singida Fountain Gate kwa ajili ya kumpata beki wa kati, Pascal Wawa kwa mkopo utakaomuweka kwenye viunga vya Mbarali hadi msimu ujao.
Ihefu FC inatumia nafasi hiyo baada ya Singida kukamilisha dili la beki wa kati, Joash Onyango kwa mkopo kutoka Simba SC ambaye inaelezwa anaenda kutengeneza pacha kali na Mkongomani, Carno Biemes.
Taarifa kutoka Singida Fountain Gate zinaeleza huenda beki huyo wakamtoa kwa mkopo ingawa maamuzi ya mwisho bado hayajafikiwa kuhusiana na suala hilo.
“Kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi chetu msimu ujao kwa sababu ya mashindano mbalimbali lakini suala la nani anatoka hadi sasa bado ni gumu kutokana na mikataba yao,” kimesema chanzo hicho.
Akizungumzia hilo Afisa Mtendaji Mkuu wa Singida Fountain Gate, Olebile Sikwane amesema wako kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji na watakapokamilisha dili zao wataziweka wazi kama ilivyokuwa utaratibu.
“Ukiangalia mchezaji tuliyetangaza kumuacha ni Miguel Escobar na tuliyemsajili ni Yahya Mbegu tu hivyo kuna mambo tunaendelea kuyakamilisha na pindi yakikamilika tutawatangazia rasmi,” amesema.
Katibu Mkuu wa Ihefu, Zagalo Chalamila amesema hawezi kuzungumzia suala la Wawa kwa sasa, kwa vile bado wanaendelea na mazungumzo ya kuwapata mastaa wapya watakaokiongezea nguvu kikosi cha timu hiyo.