Kocha mkuu wa klabu ya Ihefu, Zuberi Katwila amesema ana subiri kwa hamu dirisha dogo lifunguliwe aweze kufanya usajili wenye tija usiyopungua wachezaji watano ili kuimarisha kikosi chake ambacho hakina mwenendo mzuri katika msimu huu wa ligi kuu Tanzania bara.
Katwila ambaye alijiunga na Ihefu wiki kadhaa zilizopita baada ya kujiuzulu kuifundisha Mtibwa Sugar, bado anasota kupata ushindi katika kikosi hicho baada ya jioni ya leo kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Tanzania Prisons katika mchezo uliochezwa mkoani Rukwa.
”Ninahitaji kuongeza wachezaji wazoefu wenye uwezo mkubwa wasiopungua watano katika nafasi tofauti ili kuleta uwiano mzuri ndani ya kikosi, moja ya vitu vinavyo nigharimu ni uzoefu mdogo wa wachezaji niliowakuta kwenye kikosi” alisema Katwila.
Kikosi cha Ihefu chini ya Katwila kimecheza mechi tano, kimepata sare mbili na kufungwa mechi tatu ambapo hivi sasa kinaburuza mkia katika msimamo wa VPL kwa alama zao tano baada ya michezo kumi waliyocheza tangu kuanza kwa msimu wa 2020/21.