Wakati baadhi ya timu Ligi Kuu zikisaka maeneo nje ya mikoa yao ili kupiga kambi kujiwinda na msimu ujao, Ihefu FC imesema haina mpango wa kuondoka Mbeya, huku ikithibitisha kumalizana na makocha wake John Simkoko na Zuibery Katwila.
Ihefu imeanza kambi ya mazoezi na baadhi ya wachezaji tu chini ya kocha Zuberi Katwila na Themi Felix.
Hadi sasa timu hiyo ya wilayani Mbarali imewaongezea mikataba nyota wao, wakiwamo Jafari Kibaya, Never Tigere, Juma Nyosso, Rafael Daud, Lenny Kissu, Juma Rashid na Mlinda Lango Fikirini Bakari.
Hata hivyo tayari imeondokewa na wachezaji kadhaa wakiwa ni Andrew Simchimba (KMC), Yahya Mbegu (Singida Fountain Gate) James Ssetuba na Nico Wadada, huku ikiendelea na mazungumzo na Yacouba Songne na Obrey Chirwa.
Afisa Habari wa timu hiyo, Peter Andrew amesema tayari timu imeanza mazoezi na uongozi umemalizana na makocha kwa kuwaongezea mikataba sawa na baadhi ya wachezaji.
Kuhusu mazingira ya kambi, Andrew alisema hawatarajii kuondoka nje ya Mbeya badala yake ni aidha Tukuyu au sehemu nyingine kutokana na mapendekezo ya kocha.
“Ni kweli wachezaji wengi mikataba yao iliisha, hivyo kila mmoja anaamua kutokana na ofa na maslahi anayopata sehemu nyingine, ila wapo tuliobaki nao na ishu ya makocha wamerejea kikosini.” amesema Andrew, huku kocha Katwila akikazia kwa kusema;
“Kambi tayari imeanza tangu juzi na hatutarajii kwenda popote nje ya Mbeya, tutakuwa na mechi za kujipima nguvu, kwa wachezaji watakaochelewa kuripoti tutawachukulia hatua.”