Kocha Msaidizi wa Ihefu FC, Zuberi Katwila amesema pamoja na kutarajia upinzani mkali kutoka kwa Simba SC, lakini mipango na hesabu zao ni kushinda mchezo huo na kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Ihefu FC itaumana na Simba SC katika mchezo wa Robo Faiali ‘ASFC’ mwishoni mwa juma lijalo (April 07) katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, kabla ya kurudiana tena kwenye mchezo wa Ligi Kuu Aprili 10 kwenye uwanja wa Highland Estate Mbarali.
Timu hiyo ambayo kwa sasa imeonesha makali ikiwa haijapoteza mchezo wowote kati ya michezo minne iliyocheza mfululizo ikishinda mitatu na sare moja na kuwa nafasi ya sita kwa pointi 33, imedhamiria kushinda na kutinfa Nusu Fainali na ikiwezekana kutwaa Ubingwa wa ‘ASFC’.
Katwila amesema; “Kila timu iliyofuzu si kwa bahati hivyo hata ikitokea nafasi ya ubingwa tuko tayari na ndio lengo letu, tunaendelea kujifua kujiweka fiti kwa ajili ya mechi hiyo.”
Michezo minne mfululizo ambayo Ihefu FC imezoshinda ni dhidi ya Tanzania Prisons 2-1, Mbeya City 2-0, Dodoma Jiji 2-1 na Azam FC 1-0 huku ikitoa sare ya 1-1 dhidi ya Singida Big Stars na sasa inajiandaa kuwakaribisha Wekundu Msimbazi.