Klabu ya Ihefu FC imetangaza tahadhari kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kuelekea Mzunguuko wa Pili ambao umepangwa kuanza Desemba 15.
Ihefu FC inayojivunia kuwa timu ya kwanza kuvunja Rekodi ya Young Africans iliyocheza michezo ya 49 ya Ligi Kuu bila kupoteza tangu msimu uliopita, imepanga kupambana ili kuepuka kushuka Daraja.
Afisa habari wa Ihefu FC Peter Andrew amesema Klabu yao imejipanga kupambana na kujiondoa kwenye nafasi za mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu, kwani wamedhamiria kucheza Ligi hiyo msimu ujao wakiwa bora zaidi.
“Tumejipanga kupambana kwenye mzunguuko wa pili, tunaamini utakuwa mgumu kwa sababu ni wa kujizatiti kwa asilimia mia moja, ili kuhakikisha tunafanya vizuri na kusalia kwenye Ligi Kuu.”
“Ihefu FC ni timu nzuri na tunajua wapi tulipokosea katika Mzunguuko wa Kwanza, tumejipanga kurekebisha makosa na kuwa imara zaidi ya tulivyofanya kwenye mzunguuko wa kwanza.” amesema Peter
Ihefu FC imemaliza Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi Kuu ikiwa nafasi ya 14 katika Msimamo, ikiwa na alama 11 ilizovuna baada ya kucheza michezo 15, ikishinda mitatu, kufungwa kumi na kuambulia sare miwili.