Klabu ya Ihefu FC imefunga usajili kwa ajili ya msimu ujao, huku benchi la ufundi likipiga mkwara kuwa kazi iliyobaki ni kusubiri Agosti 15 waanze walipoishia wakisisitiza nafasi nne za juu hawakosi.
Timu hiyo licha ya kutotangaza wazi usajili mpya zaidi ya wale walioongezewa mikataba, lakini Dar24 imenasa nyota wote waliosaini kandarasi ya kukitumikia kikosi hicho msimu ujao.
Ligi Kuu inatarajia kuanza Agosti 15, ambapo Ihefu itakuwa na benchi lake lile lile la msimu uliopita chini ya kocha mkuu, John Simkoko akisaidiwa na Zuberi Katwila na Themi Felix.
Mastaa waliosajiliwa ikiwa ni ingizo jipya ni Issa Rashid, John Kitenga, Vedastus Mwihambi, Shaban Msala, Ismail Mgunda, Nassor Sadun, Mpoki Mwakinyuke na Ezekiel Mwashilindi.
Wengine ni Geofrey Manyasi, Keneth Kunambi, Rajabu Athuman, Charles Ilamfya na Victor Akpan ambaye alikuwa kwa mkopo msimu uliopita na sasa ni mali halali ya ‘Mbogo Maji’.
Katwila amesema tangu waanze kambi benchi la ufundi linaridhishwa na ubora wa mchezaji mmoja mmoja na kwamba kupitia michuano ya Mbeya Pre Season wanaamini hadi Agosti 15 kikosi kitakuwa imara.
“Tumefunga usajili, hawa waliopo naamini wanatosha na kazi yetu ni kuanza kusuka upya kwa ajili ya msimu ujao, tunaridhishwa na kile wanachoonesha kwa kuwa hakuna mtu wa majaribio na wote wanafahamu soka la ushindani,” amesema Katwila.
Amesema wataendelea kutafuta mechi nyingi za kirafiki kadri watakavyopata kuhakikisha wanapoanza Ligi Kuu msimu mpya Ihefu FC iendeleze makali yake kama ilivyokuwa msimu uliopita.