Kocha mkuu wa Ihefu FC, Zubery Katwila amesema kwa sasa hana shaka hata kidogo juu ya suala la kushuka daraja, baada ya kikosi chake kuimarika katika duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katwila ametoa kauli hiyo kufuatia juhudi za kupambana kwa wachezaji wake tangu alipofanya maboresho kwa kuwasajili baadhi yao kupitia dirisha dogo ambalo lilifungwa rasmi Januari 15.
Tayari klabu hiyo inayoshiriki kwa mara ya kwanza kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara imeshajikusanyia alama nne ugenini, katika michezo miwili waliocheza tangu mzunguuko wa pili ulipoanza.
Ihefu FC ilipata ushindi wa 2-0 ugenini katika uwanja wa mabatini Pwani, dhidi ya timu ngumu ya Ruvu Shooting iliyoko kwenye kiwango bora kwa sasa, pia wakalazimisha sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar.
Katwila amesema, ”Uelewa wa wachezaji wangu umeongezeka baada ya kukaa chini na kujadili mambo kadhaa kuhusiana na mwenendo wa ligi hasa mechi zilizobaki na umuhimu wake, pamoja na ukweli pia dirisha dogo limetusaidia kupata wachezaji wazoefu ambao wameongeza kitu kikubwa kikosini.”
”Tulianza kwa vikao vya benchi la ufundi na viongozi wa juu wa timu (wakurugenzi) wakatupa malengo machache tu, ikiwemo kuibakiza timu katika ligi kuu msimu ujao, ili tujipange upya vizuri kwa ushiriki wetu wa msimu mwingine”.
Katika msimamo wa ligi Ihefu ipo katika nafasi ya 16 miongoni mwa timu 18 zinazoshiriki ligi hiyo ikiwa na alama 17 kibindoni katika michezo 20 walioshuka dimbani, pia wanajivunia michezo 8 iliyobaki nyumbani isiyohusisha Simba, Yanga na Azam kwa kuwa walimalizana nazo duru la kwanza.