Kikosi cha KMC FC leo Jumatatu (Januari 25) kinatarajiwa kuanza maandalizi ya mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania, baada ya kuingia kambini jijini Dar es salaam tangu juma lililopita.
Afisa Habari na Mahusiano wa KMC FC Christina Mwagala amesema mbali na kuanza maandalizi ya duru la pili la Ligi Tanzania Bara inayotarajiwa kuendelea Februali 13, pia kikosi chao kitacheza michezo kadhaa ya kirafiki.
Pia amesema wachezaji ambao wamewasajili kupitia dirisha dogo la usajili Charles Ilanfya pamoja na Matheo Anthony ni sehemu ya walioanza kambi na wanatarajiwa kuanza mazoezi na wenzao chini ya kocha Mkuu John Simkoko pamoja na msaidizi wake Habibu Kondo.
“Timu ilirejea kambini tangu Januari 18, lakini kutokana na msiba wa kiongozi mwandamizi wa Timu Raphael Waryana uliotokea Januari 14 mwaka huu hatukuweza kufanya mazoezi rasmi na kwamba kilichokuwa kinafanyika ni kujiweka sawa, lakini leo tuna anza rasmi mazoezi yetu”.
Itakumbukwa kuwa wachezaji wa KMC FC walipewa siku 10za mapumziko, na sasa wote wamerejea kambini, isipokuwa wale walioitwa katika Timu ya Taifa ambao ni Juma Kaseja, Israel Patric Mwenda, na wengine ambao hawajarejea ni wale ambao wapo katika Timu ya Taifa ya Vijana U 20, David Brayson, Hassan Kapalata pamoja na Rahim Sheih.