Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Charles Ilanfya, amesema amejipanga kisawa sawa kurejea klabuni hapo, baada ya kumaliza mkataba wa mkopo wa muda mfupi, akiwa na KMC FC.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu 2020-21 akitokea KMC FC, alilazimika kurejeshwa kwa mkopo kwenye klabu hiyo ya Kinondoni, kufuatia kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Msimbazi.
Ilanfya amesema amejipanga kurejea kwenye kikosi cha Simba SC na kupambania nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, kutokana na kuamini ana uwezo wa kufanya hivyo, baada ya kujifunza mambo mengi akiwa nje kwa mkopo.
“Bado nina mkataba na Simba SC, mkataba wangu wa mkopo KMC FC umemalizika leo (juzi), hivyo narudi Simba SC na wao ndio wataamua hatima yangu.”
“Najua sasa Simba SC wana washambuliaji bora ambao kila mmoja kwa nafasi yake anafanya vizuri, lakini sio kigezo cha kushindwa kurudi pale na kufanya, vizuri kwani uwezo ninao na nitaenda kuipambia Simba ” amesema Ilanfya.
Kurejea kwa Ilanfya Simba SC, ni dhahir anakwenda kupambania nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza dhidi ya Nahodha John Bocco, Meddie Kagere na Chriss Mugalu, ambao wamemaliza msimu wakiwa kwenye nafasi za juu katika orodha ya wafungaji bora msimu wa 2020-21.