Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba SC Imani Kajula ameanika hadharani mpango mkakati wa kazi zitakazofanywa na klabu hiyo ili kufikia malengo ndani na nje ya Tanzania.
Kajula alitangazwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu Simba SC katikati ya juma hili akichukua nafasi ya Barbara Gonzalez aliyejiuzulu mwishoni mwa mwaka 2022.
Wakati akitangaza mpango mkakati huo, Kajula aliwataka Wanachama wa Simba SC kumpa ushirikiano ili kufanikisha kinachokusudiwa klabuni hapo.
“Mimi sio CEO, mimi ni CCO, kazi yangu ni kuwaunganisha. Ningependa mnichukulie kazi yangu kuwa kiunganishi kuliko kuwa kiongozi.”
“Kwa namna ya kipekee nimshukuru sana Barbara Gonzalez, jana alinipigia simu, kesho tutaongea na Jumatano ijayo tutakutana ili kuwa na mwendelezo mzuri.”
“Ninyi ndio roho ya Simba (wanachama), bila ninyi hakuna Simba. Cha kwanza ni kuhakikisha tunaboresha mawasiliano, kuhakikisha tunawasikiliza.”
“Tutaimarisha matawi, sana tu, tutajenga mfumo endelevu, miaka ijayo tutafanya mkutano wa kiteknolojia kwa kushirikisha watu wote nchi nzima.”
“Tunataka tushinde, lazima kujenga timu bora lakini kazi ya pili ni kujenga taasisi imara na endelevu hata nisipokuwepo kuwe na mtu mwingine wa kuendeleza. Lakini pia kujenga chapa imara, tunayo lakini kuongezea mapato.”
“Kwenye Ligi ya Mabingwa (wanaume) tunataka kufanya vizuri, timu yetu ya wanawake imefanya vizuri sana Afrika.”
“Lazima tuongeze wadhamini wengine, kati ya kazi yangu ni kwenda kuwatembelea wadhamini wetu.”
“Lengo la timu yetu ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu, lakini Ligi ya Mabingwa Afrika kufika robo fainali au zaidi. Simba Queen SC kufanya vizuri zaidi Afrika na kuboresha timu za vijana.” amesema Imani Kajula.