Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Imani Kajula amewahimiza Mashabiki wa Soka bila kujali itaikadi zao, kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, siku ya Jumamosi (April 22).
Simba SC itacheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wydad Casablanca, ikidhamiria kuweka rekodi ya kutinga Nusu Fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Imani ametoa wito huo alipozungumza na Waandishi wa Habari leo Jumanne (April 18), katika ofisi za Simba SC Masaki jijini Dar es salaam, huku akiamini siku ya Jumamosi (April 22) itakua na Baraka, hivyo kutakuwa na kila sababu ya kikosi chao kufanya vizuri.
“Mechi itachezwa siku yenye baraka, naomba kuwakaribisha Watanzania wote kuja kuangalia timu mbili bora zikicheza.”
“Lengo letu ni kuwa klabu ya michezo bora barani Afrika. Tunaendelea kuboresha hilo kwa kuwa moja ya timu bora 10 Afrika na ndio timu pekee Tanzania ambayo itacheza CAF Super League.”
“Tunawashukuru wadhamini wetu M-Bet kwa ushirikiano ambao wanatupatia. Leo watatukabidhi kishika mkono kwa kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.” amesema Imani Kajula
Wakati huo huo Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema mchezo wao dhidi ya Wydad Casablanca umepangwa kuanza mishale ya saa kumi jioni, tofauti na ilivyokuwa katika michezo ya Hatua ya Makundi, ambayo walicheza usiku.
“Kikubwa ni kuelezea maandalizi yetu kuelekea mchezo dhidi ya Wydad AC.”
“Mechi yetu dhidi ya Wydad AC itakuwa ni Jumamosi Aprili 22, 2023 saa 10:00 jioni. Mnakumbuka mechi za makundi tulicheza saa 1 usiku lakini mechi hii tumepata saa 10 na hilo ni baada ya kuwaomba CAF sababu itakuwa sikukuu ili kila Mwanasimba aje uwanjani.”
“Baada ya kumnyoa mtani jana wachezaji walipata muda wa kupumzika na leo wameingia kambini na saa 10 jioni wataanza mazoezi kwenye uwanja wetu wa Mo Simba Arena.”
“Kuhusu majeruhi, Kanoute anasumbuliwa na nyonga na leo atawasili kambini kukutana na madaktari kama atakuwa sawa ataanza mazoezi, hivyo hivyo kwa Aishi Manula atakutana na madaktari kuangalia hali yake.”
“Mechi yetu itakuwa na VAR maofisa wake watafika kesho. Wydad AC na wao watafika kesho saa 5 asubuhi wakiwa na msafara wa watu 50 na watakuja na ndege ya kukodi. Waamuzi na wao watafika nchini kesho.” amesema Ahmed Ally