Wakati Simba SC ikikabiliwa na michezo miwili ya kukamilisha msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa klabu hiyo umebainisha watafanya mapinduzi yakayosaidia timu yao kutimiza malengo yake katika msimu mpya wa mwaka 2023/24.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC iko kwenye nafasi ya pili ikiwa na alama 67 huku watani zao Young Africans wenye alama 74 kibindoni wameshatangazwa mabingwa wapya wa msimu huu, kila timu ikibakisha mechi mbili kumaliza msimu.
Kikosi cha Mnyama sasa kinaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena chini ya Kocha Mkuu Robert Oliveira ‘Robertinho’ kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Polisi Tanzania utakaopigwa Jumanne na baadaye itafunga pazia kwa kuwakaribisha Coastal Union Juni 9, mwaka huu.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula, amesema wakati klabu inajipanga kuhakikisha wanaimarisha kikosi lakini pia wanahitaji kumaliza msimu kwa kuwapa furaha mashabiki wao kwa kushinda mechi hizo mbili.
Kajula amesema watafanya kazi kubwa kwenye maboresho ya kikosi kwa kuwaongeza wachezaji wazuri ambao watatoka katika klabu zilizofanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
“Tumekutana na kocha wetu Robertinho ambaye ameweka mezani mapendekezo yake ya awali ya usajili kabla ya kutukabidhi ripoti ya msimu baada ya ligi kufikia tamati.
“Tunatambua haukuwa msimu mzuri kwetu, tunajua tulipojikwaa na tunachokifanya kwa sasa ni kuangalia pale tulipokwama, kuboresha kwa ajili ya kupata matokeo chanya katika mashindano tutakayoshiriki msimu ujao,” amesema mtendaji huyo.
Ameongeza mapungufu yote yaliyotokea msimu huu yanafanyiwa kazi kwa sababu wanafahamu katika mpira unatakiwa kujiimarisha ili urejee ukiwa imara na tayari kupata matokeo chanya.