Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka waajiri nchini kuchukua hatua za kuimarisha mifumo ya kuwalinda wafanyakazi wao dhidi ya vihatarishi vilivyomo katika maeneo yao ya kazi, ikiwemo kuwa na mwongozo wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, kufanya tathmini ya vihatarishi mahali pa kazi, Kuhakikisha wafanyakazi wao wanapimwa afya.
Majaliwa, ameyasema hayo wakati wa kuahirisha Mkutano Wa 12 wa Bunge jijini Dodoma na kuongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kubaini athari ya vihatarishi kwa mfanyakazi na kuhakikisha maeneo yao yanafanyiwa kaguzi za usalama na afya ili kuwalinda wafanyakazi na uwekezaji wao.
Amesema, Wafanyakazi wanatakiwa pia kuhakikisha wanazingatia taratibu na miongozo ya kujilinda dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali au magonjwa wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao. Hii itasaidia kulinda afya na usalama wao pamoja na kumpunguzia mwajiri gharama za uendeshaji pale wanapougua au kupata ajali wakiwa kazini.
Aidha, Majaliwa pia amesema Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uongeze wigo wa kutoa elimu kwa wafanyakazi ili watambue huduma zinazotolewa na mfuko huo. Vilevile, waajiri watumie ipasavyo mifumo ya TEHAMA kupata huduma, kujisajili na kuwasilisha kwa wakati michango katika mfuko huo.