Mamilioni ya watu wanadaiwa kuishiwa na Chakula nchini Sudan, na baadhi yao wanafariki kutokana na ukosefu wa huduma za afya, ikiwa miezi minne ya vita imepita ambapo mji mkuu wa Khartoum na vitongoji vyake vikiharibiwa kufuatia mashambulizi ya kikabila ya kuwania madaraka.
Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu, Elizabeth Throssell, ame sema katika kikao fupi mjini Geneva kuwa, “miili ya watu wengi waliouwawa haijakusanywa, kutambuliwa au kuzikwa,” lakini Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 4,000 wameuawa.”
Zaidi ya watu milioni nne wamekoseshwa makazi, wakiwemo takribani watu milioni moja ambao wamekimbilia nchi jirani huku raia katika majimbo yaliyoathiriwa na vita wakiuawa katika mashambulizi hayo wengine bila kugundulika na waliojeruhiwa kukosa msaada.
Mzozo kati ya jeshi la Sudan na jeshi la Vikosi vya Msaada wa Dharura – RSF, uliozuka Aprili 15, 2023 unadaiwa unatokana na mivutano inayohusishwa na mpango wa mpito kurejesha utawala wa kiraia, ambao umeitumbukiza nchi katika ghasia na kusababisha ukosefu wa uthabiti katika eneo hilo.