Umoja wa Mataifa – UN, umesema idadi ya vifo vya raia vilivyothibitishwa nchini Ukraine tangu Russia ilipovamia nchini humo inakaribia kufikia watu 8,500, huku ikihisiwa idadi halisi ni kubwa zidi ya ile iliyotangazwa.
Taarifa ya Ofisi ya Kamishna mkuu wa Umoja wa mataifa wa haki za binadamu, ilisema pamoja na waliouawa, imethibitika kuwa pia zaidi ya raia 14,000 walijeruhiwa kutokana na mashambulizi mbalimbali ma kusababisha vilema vya maisha au makovu.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, “OHCHR inaamini kwamba takwimu halisi ni kubwa zaidi kwani upokeaji wa taarifa kutoka maeneo ambapo mapigano makali yamekuwa yakiendelea umecheleweshwa, na ripoti nyingi bado zinasubiri kuthibitishwa.”
Aidha, UN imesema katika siku tisa za kwanza za mwezi Aprili vilithibitishwa vifo vya raia 44, huku mashambulizi ya Russia kwa miezi ya hivi karibuni nchini Ukraine yakilenga miundombinu ya nishati na Kyiv ilisema majaribio hayo ni ya kuwakatisha tamaa Waukraine kwa kukata umeme na maji katika nyumba na biashara zao.