Watu zaidi ya 10 wameuawa na wengine wapatao 150 wamejeruhiwa jana katika makabiliano kati ya waandamanaji wa makundi yanayokinzana mjini New Delhi nchini India.
Makabiliano hayo ni mabaya zaidi kushuhudiwa tangu vurugu zilipozuka juu ya sheria mpya ya uraia mwanzoni mwa mwezi Desemba.
Vurugu hizo zilianza tangu mwishoni mwa juma lakini ziligeuka kuwa mbaya zaidi Jumatatu iliyopita.
Imeelezwa kuwa machafuko mapya yalianza tena jana Jumanne katika maeneo tofauti ya mji mkuu huo wa New Delhi.
Afisa wa idara ya kukabiliana na majanga ya moto ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba timu yake imekuwa ikipokea simu za dharura za kwenda kuzima moto katika maeneo tofauti.
Sheria hiyo mpya iliyozua ghasia inawapa fursa wahamiaji wasio Waislamu kutoka nchi tatu jirani kupata urai wa India, Waislamu nchini India wanadai kuwa ni sheria ya kibaguzi.