Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe wanatarajiwa kuwasili nchini leo Jumatano (Oktoba 18) kwa ajili ya uzinduzi wa mashindano ya Ligi ya Afrika, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam keshokutwa Ijumaa (Oktoba 20).
Infantino na Motsepe watashuhudia mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo kati ya Simba SC ya Tanzania na Al Ahly ya Misri siku hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay amesema wanatarajia kupokea ugeni wa viongozi wa soka wapatao 250 kuanzia leo Jumatano (Oktoba 18).
Amesema ugeni huo utajumuisha wakuu wa idara mbalimbali za mashirikisho hayo, marais wa vyama na mashirikisho ya soka ya nchi zote Afrika pamoja na marais waalikwa wa mashirikisho ya mabara mengine.
“Marais wote wa vyama na mashirikisho ya soka Afrika watakuwepo, sekretarieti ya CAF itakuwepo, maofisa wa FIFA watakuwepo,” amesema Mayay.
Amesema Serikali imefanya maombi katika hoteli zote kubwa na zimeshajaa na wanategemea kuwa na shughuli kubwa ambayo imebeba watu wakubwa katika mpira wa miguu duniani, hivyo ni faraja na fahari kwa taifa kupokea ujumbe mkubwa kama huo.
Mbali na ujo wa wageni hao wapinzani wa Simba SC katika mechi hiyo, Al Ahly wanatarajiwa kuingia leo.