Wakati Simba SC ikielekea mkoani Lindi tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 22 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC, Beki wa klabu hiyo kutoka Henock Inonga amefunguka kazi kubwa aliyoifanya Jumamosi (April 30), kwa kumzuia Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Kalala Mayele.
Inonga alikua na mchezo mzuri Jumamosi, na alionekana kuzikonga nyoyo za mashabiki wa Simba SC, amesema alilazimika kuhakikisha anakuwa makini na Mayele ili kutompa nafasi mshambuliaji huyo kutikisa nyavu zao halafu ‘akatetema’ mbele yake.
Inonga amesema alifanikiwa kumzuia na hakuweza kutetea na kwamba licha ya mchezo huo kuwa mgumu kwa kila upande, lakini malengo yake ya kutompa nafasi mshambuliaji huyo kutimiza ahadi yake yalifanikiwa kwa asilimia 100.
“Tumepambana, malengo yalikuwa alama tatu, lakini tumepata moja ila nimefanikiwa kumzuia mtu asiteteme (No kutetema), licha ya kutoka nchi moja na kuonyesha ni mechi ya upande wetu hakuweza kutetema,” amesema Inonga.
Mayele ndiye kinara wa mabao hadi sasa kwenye Ligi Kuu msimu huu, akiwa amecheka na nyavu mara 12 akifuatiwa na George Mpole wa Geita Gold FC mwenye mabao 11.
Kwa matokeo ya mchezo wa Jumamosi (April 30), yanaifanya Young Africans kufikisha alama 55 kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakati huu ikibakiza michezo tisa kabla ya kufunga msimu huu, hata hivyo inafutiwa na Simba SC yenye alama 42, lakini ikicheza mchezo moja pungufu.
Simba itashuka tena dimbani kesho Jumanne (Mei 03) Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi kuwavaa wenyeji wao, Namungo FC waliopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na alama zao 29 zilizotokana na michezo 21.