Simba SC imeendelea na maandalizi ya kuikabili Al Alhy ya Misri kwenye mechi ya uzinduzi wa michuano mipva ya African Foothall League itayopigwa Oktoba 20, Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini taarifa njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kupona kwa nyota tegemeo beki Henock Inonga na kipa Aishi Manula.

Manula alikuwa nje ya uwanja tangu mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kufanyiwa upasuaji wa nyonga, lakini kwa sasa yuko tayari kwa mechi na jana jumatano (Oktoba 11) alifanya mazoezi na wenzake huku Inonga aliyeumia kwenye mechi ya ligi dhidi ya Coastal Union, Septemba 21, katika Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam akiwa amepona na tangu juzi jumatatu (Oktoba 09) anashiriki mazoezi ya timu ya taifa ya DR Congo inayojiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya New Zealand itakayopigwa kesho Ijumaa (Oktoba 13) nchini New Zealand.

Tangu Manula alipoumia katika eneo la kipa wamekuwa wakidaka kwa kupokezana Ally Salim na Ayoub Lakred, lakini wameshindwa kuonyesha umwamba kama Manula jambo lililozua hofu kwa baadhi ya mashabiki ambao hawawaamini makipa wawili hao na wengine waliopo Ahmed Feruz na Hussein Abel kama ilivyo kwa beki Kennedy Juma aliyetumika mbadala wa Inonga.

Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amefurahishwa na maendeleo ya Manula na Inonga na kuthibitisha kuwepo kwenye mipango yake, lakini akiwataka kuendana na kasi ya kikosi ilivyo.

Robertinho amewataja Inonga na Manula kama wachezaji wazoefu Simba SC na wamekuwa na faida kubwa wanapokuwa uwanjani hususan kwenye mechi zinazohitaji uzoefu.

“Ni wachezaji wazuri, nafurahi kuona wakiendelea vyema kwani uwepo wao ni faida kwetu kutokana na uzoefu na uwezo wao mkubwa wawapo uwanjani. Bado sijaamua kuwatumia au kutowatumia kwenye mechi na Ahly, lakini wapo kwenye mipango na kitakachowapa nafasi ni kuendana na kasi na namna timu itakavyokuwa inahitaji kucheza. Bado sijaamua kuwatumia au kutowatumia kwenye mechi na Ahly lakini wapo Ikwenye mipango.” amesema Robertinho.

Wakati Simba SC ikiendelea na mazoezi ya mechi hiyo kwenye uwanja wake wa Mo Simba Arena, Bunju, Dar es salaam inatarajia kucheza mechi mbili na timu mbili za madaraja ya kati kabla ya kuivaa Ahly.

Wakati huohuo Simba SC imeendelea na mazungumzo na Shirikisho la Soka la Zambia anakotokea kiungo Clatous Chama, DR Congo kwa kina Inonga na Tanzania, ili kuwapa muda wa kutosha wachezaji walioitwa kwenye vikosi vya timu hizi za taifa ambao wameitwa hivi karibuni kwa ajili ya mechi za kimataifa katika dirisha hili.

Kocha KMC FC afichua siri ya mafanikio
Harry Kane kutembelea nyota ya Ronaldo, Messi