Kiungo Mshambuliaji wa Coastal Union Hija Ugando amemuomba radhi Beki wa Simba SC Henock Inonga Baka kwa kitendo kisicho cha kiungwana alichomfanyia wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa jana Alhamis (Septemba 21), Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Ugando alimchezea rafu Beki huyo kutoka DR Congo iliyosababisha kutolewa nje kwa kadi nyekundu, huku Inonga akikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Temeke.
Akiomba radhi kwa tukio hilo Ugando amesema hakudhamiria kumchezea vibaya Inonga, na siku zote kwani yeye si muumini wa vitendo hivyo.
“Binafsi imeniumiza sana, na nimesikitika. Sijawahi kufanya kitendo kile kabla. Ninamuomba radhi mchezaji mwenzangu, mwanafamilia mwenzangu (Inonga).”
“Sikudhamiria, mimi si muumini wa kufanyiana vitendo vibaya. Mimi ni muumini wa watu kufanyiana Fair” ameema Haji Ugando amezungumza baada ya mchezo ulioisha kwa timu yake kupoteza kwa goli 3-0.
Wakati huo huo Daktari wa Hospitali ya Temeke Richard Jomba ameelezea hali ya jeraha la mlinzi wa Simba SC, Henock Inonga aliyepata jeraha katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ambapo amebainisha kuwa jeraha lake sio kubwa na kwamba hatakaa nje kwa muda mrefu.
“Kwa ujumla mpaka sasa hivi kwa hatua hii mpaka natoka, haki yake ni nzuri na jeraha lake sio kubwa, ni dogo na vitu vyote vimeshafanyika na yuko vizuri, sasa yupo kwenye mapumziko mafupi na ataruhusiwa kutoka hapa hospitali.”
“Kwa vipimo vya haraka haraka alivyofanyiwa sidhani kama atakaa nje kwa muda mrefu, kilichobakia ni kuuguza sehemu ya kidonda Kwa hiyo atakuwa na muda wa kuuguza ile ngozi ile sehemu ya kidonda lakini si vinginevyo.” amesema Dkt Jomba