Klabu ya Inter Milan ya Italia ipo tayari kumsajili kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Croatia Luka Modric, lakini imesisitiza kusubiri baraka zitakazotolewa na uongozi wa Real Madrid.
Inter Milan wamethibitisha kuwa tayari kukamilisha mpango wa usajili wa kiungo huyo, baada ya kujiridhisha yupo tayari kuondoka Santiago Bernabeu katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.
Rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez anatarajiwa kukutana na viongozi wa Inter Milan ili kufanya mazungumzo ya uhamisho wa kiungo huyo, ambaye tayari ameshakataa kusiani mkataba mpya.
Kwa mujibu wa gaezti la michezo la Italia (Gazzetta dello Sport), Uongozi wa Inter Milan upo tayari kumlipa mshahara Modric wa Euro milioni 10 kwa mwaka, tofauti na mshahara wake wa Euro milioni 6.5 anaoupokea kwa mwaka akiwa Real Madrid.
Tayari vikao vya ndani vya uongozi wa klabu hiyo ya mjini Milan vimeshaafiki mshahara huo, na kinachosubiriwa ni mazungumzo ambayo yatabariki uhamisho wake.
Gazeti hilo limeongeza kuwa, huenda rais wa Real Madrid, akakutana na uongozi wa Inter Milan kesho Jumamosi, na kuna uwezekano wa kupatikana kwa muafaka wa uhamisho wa Modric kabla ya kuanza kwa juma lijalo.
Katika hatua nyingine Inter Milan imejiandaa kuwasajili Sergej Milinkovic kutoka Lazio na Christian Eriksen Tottenham Hotspur, katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.