Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), limesikitishwa na vifo vya wahamiaji wasiopungua 20 vilivyotokea katika jangwa la nchi ya Libya na kutoa wito kwa Taifa hilo na nchi ya Chad kuchukua hatua za ziada katika kuwalinda wahamiaji kwenye mpaka wa nchi hizo.
Taarifa ya IOM kutoka Geneva nchini Uswisi, inasema shirika la huduma ya afya ya dharura la Libya Juni 28, 2022 lilikuta miili ya watu 18 wanao aminika kuwa raia wa Chad na wa Libya karibu na mpaka wa nchi hizo mbili ambao wanaaminika vifo vyao vilitokana na kiu wakiwa jangwani.
Mkuu wa IOM nchini Libya, Federico Soda amesema “Vifo vya watu 20 katika jangwa la Libya utumike kama wito mwingine wa kuamsha jumuiya ya kimataifa na ukumbusho kwamba tuko mbali sana kufikia lengo la ‘kutomwacha mtu nyuma’, la malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa kufikia mwaka 2030.”
Aidha, Soda mekumbusha kuwa hasara inayopata Dunia kupitia vifo vinavyotokea katika Bahari ya Mediterania na katika majangwa ya kusini mwa Libya hazikubaliki na zinaweza kuepukika.
Kwa upande wake, Mkuu wa IOM nchini Chad, Anne Kathrin amesema tangu kuimarishwa kwa uchimbaji wa dhahabu kaskazini mwa nchi ya Chad mwaka 2012, eneo la mpaka wa nchi hiyo na Libya limekuwa na ongezeko kubwa la matukio yanayohusiana na wahamiaji kutelekezwa na wafanyabiashara na wasafirishaji, au wasafirishaji kupotea.
Mapema mwezi Juni 2022, mapigano kati ya wachimba madini wa dhahabu yaliyotokea mji wa Kouri Bougoudi, uliopo jirani na mpaka na Libya, yalisababisha mamia ya watu kupoteza maisha na takriban wafanyakazi 10,000 wa migodini kaskazini mwa Chad waliyakimbia makazi yao.
Zaidi ya wahamiaji 45,000 walirekodiwa katika Vituo vya Ufuatiliaji vya wahamiaji vya Faya, Zouarké na Ounianga Kébir vilivyopo Kaskazini mwa Chad kati ya Januari na Machi 2022, huku miongoni mwa wahamiaji waliohojiwa na IOM katika kipindi hicho, wakisema asilimia 32 kati yao walielekea Libya.