Mkuu wa shirika la kudhibiti uundaji wa silaha za nyuklia duniani amethibitisha kuwa Iran imeongeza uzalishaji wa madini ya uranium.
Mkuu huyo wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA, Yukiya Amano amesema kuwa haijabainika wazi kama watafikia kilichokubaliwa katika mkataba wa Kimataifa wa mwaka 2015.
Mwezi uliopita Iran ilitangaza kuwa itajiondoa katika mkataba wa nyuklia kama hatua ya kulipiza kisasi vikwazo ilivyowekewa na Marekani. huku Amano akisema anahofu kubwa kuhusu taharuki iliyopo sasa kuhusu suala la mpango wa nyuklia wa Iran na kutoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo.
Aidha, Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amesema kuwa hali ya taharuki na kuongezeka kwa mgogoro huo inaweza kupunguzwa kwa kukomesha kile alichokitaja kuwa vita vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya taifa hilo.
“Wale wanaoendeleza vita kama hivyo wasitarajie kuwa watakua salama, na kama mgogoro huu wanataka uishe basi Marekani aondoe vikwazo vya kiuchumi alivyoiwekea Iran,” alisema Javad jijini Tehran wakati wa ziara ya waziri wa mambo yya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas
Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas ameonya kuwa hali katika eneo hilo inaendelea kuwa tete na kwamba huenda ikasababisha makabiliano ya kijeshi kati ya Marekani na Iran.