Waziri wa Mambo wa nchi za Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif ameziomba China na Urusi kuchukua hatua madhubuti kuulinda mkataba wa nyuklia wa mwaka wa 2015 huku akionya kuhusu kuwepo hali hatari kutokana na ongezeko la mvutano na Marekani.
Ameyasema hayo wakati akizungumza katika wa mkutano na wa waziri mwenzake wa China, Wang Yi jijini Beijing, ambapo Zarif amesema Iran na China zinapaswa kuwa pamoja na kushirikiana kuhusu kuweka utaratibu wa dunia unaoyahusisha mataifa mengi na kuepusha utaratibu unaoletwa na upande mmoja.
Aidha, Marekani imepeleka Manowari zake za kivita katika Ghuba ya Uajemi, katika kile ambacho maafisa wa Marekani walisema kuwa ni jibu la picha zilizoionyesha Iran ikiwa imeyaweka makombora kwenye maboti madogo.
Hata hivyo, Marekani imewaamuru wafanyakazi wake wasio wa majukumu ya dharura kuondoka katika ubalozi wake wa Iraq, wakihofia mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wa Kishia ambao wana mahusiano na Iran.