Iran imepanga kurejea mpango wake wa nyuklia kwa madai kuwa Marekani na nchi washirika wameshindwa kutimiza ahadi zao kwa mujibu wa makubaliano ya mwaka 2015.
Akitoa hotuba yake kupitia kituo cha runinga cha taifa, Rais wa nchi hiyo, Hassan Rouhani amesema kuwa mbali na Marekani, nchi nyingine ambazo ni watia saini wa makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, China na Urusi hawajafanyia kazi ipasavyo makubaliano hayo.
Rais huyo ameeleza kuwa anazipa nchi hizo siku 60 kutekeleza kwa ufasaha ahadi zao vinginevyo ataachana na mpango huo ili nchi yake iendelee na mpango wake wa Uranium.
“Tunahisi kama mpango wa makubaliano wa nyuklia unahitaji kufanyiwa upasuaji na kupewa vidonge vya maumivu, yale ya mwaka jana hayakufanya kazi ipasavyo. Upasuaji huu ni kwa ajili ya kuokoa mpango huu au kuumaliza kabisa,” alisema Rais Rouhani.
Uamuzi huo umekuja ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais wa Marekani, Donald Trump atangaze kuiondoa nchi yake kwenye sehemu ya mpango huo.
Tangu wakati huo, Marekani imekuwa ikirejesha vikwazo vya kiuchumi vilivyokuwa vimeondolewa dhidi ya Iran, ingawa nchi hiyo ilikuwa ikiendelea kutii masharti ya mpango wa makubaliano, kwa mujibu wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa. Rais Trump alikosoa mpango huo ulioingiwa wakati wa utawala wa Barack Obama akiuelezea kuwa ni kosa kubwa lililofanyika.
Rais wa Iran ameeleza kuwa kama nchi hizo tano hazitasimamia ahadi yake ya kulinda mafuta na gesi za nchi hiyo, mpango huo kwao hautakuwa na maana yoyote.