Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka, Irene Uwoya na Steve Nyerere kufika katika ofisi za Baraza hilo siku ya leo, Julai 17, 2019.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza amesema kuwa wameamua kumuita msanii wa filamu nchini, Irene Uwoya pamoja na Steve Nyerere, kufuatia kitendo chao cha kuwarushia fedha Waandishi wa Habari wakati wa Kikao cha Julai 15.
Akizungumza jana Julai 16, Mngereza amesema kuwa kufuatia wito huo, wao kama Baraza hawajapanga kuwachukulia hatua zozote zile za kisheria.
”Wajibu wa baraza ni kukaa na wasanii, halafu kuzungumza nao, na baraza linafanya kazi kwa mujibu wa sheria lililoziweka na kama uliona yale ni masuala ya fedha”, amesema Mngereza.
Hata hivyo, kupitia ukurasa wa intsagram, Irene Uwoya amewaomba radhi waandishi kufuatia kitendo hicho kilichopelekea baadhi ya waandishi kuharibu baadhi ya vifaa vyao kutokana na vurugu zilizotokea wakati wa kudaka fedha hizo alizokuwa anarusha.
Amesema kuwa hakufanya hivyo kwa lengo la kudhalilisha waandishi wa habari kama ambavyo imetafsiriwa na watu wengi, kwani dhahiri anatambua umuhimu mkubwa wa waandishi wa habari katika jamii.
”Kama binadamu moyo wangu ulijawa na upendo na furaha iliyopitiliza ndipo niliona niweze kushiriki nanyi furaha hiyo kwa aina ile ya kuwatunza pesa, sababu mara nyingi mmekuwa watu muhimu katika kazi na mambo yote yanayohusu sanaa yetu na jamii kwa ujumla, na baadhi ya waandishi ambao kwa bahati mbaya waliharibu vifaa vyao wakati wa kuokota shukrani yangu (pesa) naomba mniwie radhi na mnisamehe sana na poleni sana kwa changamoto”. amesema Uwoya.
Aidha kwa upande wake, Steve Nyerere amekiri kupokea taarifa hizo na kwamba yeye kama msanii na BASATA ni Serikali, hivyo atafika kama alivyotakiwa.
Aidha Steve alipoulizwa kuhusu kitendo cha Irene Uwoya kuwatupia waandishi wa habari pesa, amejibu ”No Comment”.