Wakati Kocha wa Young Africans Nasreddine Nabi, akihusishwa kutakiwa na timu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Rais wa Klabu hiyo Mhandisi Hersi Saidi, amekwepa kuzungumzia taarifa hizo huku akimpongeza kocha huyo kwa kazi kubwa aliyoifanya msimu huu.

Nabi raia wa Tunisia, anahusishwa kuwaniwa na Kaizer Chiefs kutokana na ubora aliyouonyesha ndani ya Young Africans msimu huu.

Kocha huyo aliyetua Young Africans mwaka juzi, tayari ameshatwaa mataji ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Ngao ya Jamii na Kombe la FA katika misimu miwili mfululizo.

Mbali na kutetea mataji hayo Nabi msimu huu, aliisaidia timu yake kufika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAFCC) na kumaliza nafasi ya pili dhidi ya USM Alger.

Hata hivyo, Nabi amesema hivi sasa ni wakati wa kusherehekea mafanikio waliyopata msimu huu na kama kutakuwa na jambo lolote ataliweka wazi baadae.

“Kitu kikubwa hivi sasa ni sherehe za ubingwa na mashabiki wetu na wapenzi wa Young Africans. Kitakachokuja mbele tutakijua baadae, kwasasa tusherehekee tusherehekee ubingwa,” amesema.

Akizungumzia tetesi za kocha huyo kuhusishwa kuondoka Young Africans, Hersi alikwepa kuzungumzia huku akisema anayejua yajayo ni Mungu.

“Kwa kweli anayejua ya kesho ni Mungu pekee, mimi siwezi kuzungumzia ndoto wakati jambo hilo bado halijatokea,” amesema.

Hata hivyo, Hersi amempongeza Nabi kwa ubora aliouonyesha msimu huu na kuiongoza Young Africans kufanya vyema zaidi tofauti na ilivyokuwa awali.

“Nichukue fursa hii kumpongeza Nabi na benchi la ufundi, mipango ya mbinu ilikuwa bora sana msimu huu hatimaye tumefanikiwa kutetea mataji matatu na kucheza fainali za Kombe la Shirikisho Barani Afrika,” amesema Vilevile, Hersi amesema kikosi hicho kimezidi matarajio kiliyoyapanga watajipanga zaidi kuhakikisha msimu ujao wanafanya vyema zaidi.

PSG yanawa mikono kwa Kyllan Mbappe
Bajeti mpango wa nchi WaterAid zaidi ya Bilioni 45