Klabu ya Simba SC inahusishwa na mpango wa kumsajili kiungo kutoka nchini Burkina Faso na Klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco Ismael Sawadogo.
Simba SC inatajwa kuwa kwenye mpango huo na huenda ikakamilisha Dili la usajili wa Kiungo huyo kabla ya kufungwa kwa Dirisha Dogo la usajili Jumatatu (Januari 16).
Usajili wa Sawadogo ni pendekezo la Kocha Mkuu wa sasa wa Simba SC Robertinho, ambaye ameutaka Uongozi wa Klabu hiyo kuboresha safu ya Kiungo na Ushambuliaji, kabla ya kuendelea kwa Ligi Kuu na kuingia kwenye Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Usajili wa Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26, unahatarisha nafasi ya Kiungo kutoka nchini Nigeria Victor Akpan katika kikosi cha Simba SC, licha ya mwenyewe kupinga maamuzi hayo, akiamini bado ana uwezo wa kushindania nafasi ya kucheza Msimbazi.
Akpan amekuwa na wakati mgumu wa kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Simba SC, tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Coastal Union.
Hata hivyo Taarifa zinaeleza kuwa huenda akatolewa kwa Mkopo katika moja ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, ili kulinda kipaji chake, sambamba na kulishaiwshi Benchi la Ufundi la Simba SC kumrudisha mwishoni mwa msimu huu.