Aliyekuwa mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amekosoa uamuzi wa klabu ya Simba kuachana na kocha wake Joseph Omog na kusema hiyo ni sababu mojawapo ya klabu hiyo kuboronga katika michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.
Simba ilimfungashia virago kocha huyo raia wa Cameroon mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuvuliwa ubingwa na kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) na timu ya Green Warriors ya ligi daraja la pili.
Rage ambaye amezungumza kama mwanachama wa kawaida Simba, amesema klabu hiyo haikupaswa kumtimua kocha huyo katika kipindi ambacho timu ilikuwa inaelekea kwenye mashindano hasa mashindano muhimu kama ya Kombe la Mapinduzi.
Amesema kumuachia kocha msaidizi timu ikiwa inaelekea kwenye mashindano ni kosa, na kuongeza kuwa endapo Simba ilikuwa na mpango wa kumtimua kocha huyo, ilitakiwa kupata kwanza kocha mpya wakati Omog akiendela na kazi.
Akimzungumzia Omog, Rage amesema ni kocha mwenye uwezo mkubwa na rekodi zake zinajieleza katika vilabu mbalimbali barani Afrika na hata katika klabu ya Simba, hivyo uongozi ulipaswa kulinda heshima ya kocha huyo badala ya uamuzi aliouita wa haraka.