Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC Ismail Aden Rage anaamini Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wana nafasi kubwa ya kuitoa Al Hilal na kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Miamba hiyo ya Afrika Mashariki na Kati itakutana Jumamosi (Oktoba 08), katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kabla ya kupapatuana mjini Khartoum-Sudan kati ya Oktoba 14-16.
Rage ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Tabora mjini, amesema anaamini Young Africans ina kikosi bora na imara ambacho kina uwezo wa kucheza na yoyote Barani Afrika kwa sasa, hivyo hana budi kuipa nafasi ya kuibuka shujaa mbele ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal.
Amesema ili ufanye vizuri katika michuano ya vilabu Barani Afrika, ni lazima uwe na kikosi chenye sifa ya kupambana kama Young Africans, hivyo amesisitiza kuwa na imani kubwa na Wananchi kuelekea mchezo wa Jumamosi (Oktoba 08).
“Sioni sababu yoyote kwa Young Africans kushindwa kufanya vizuri mbele ya Al Hilal, tuwe wakweli wenzetu wana timu nzuri sana msimu huu, ninaamini timu yao itashinda Jumamosi dhidi ya hawa wasudan, ninaliweka wazi hili kwa sababu mimi sio shabiki wa mpira mimi ninapenda mpira na siamini katika itikadi za ushabiki.”
“Unajuwa katika Michuano ya Afrika ukiwa na kikosi bora na imara huna wasiwasi wa kuanza kuhofia umepangwa na nani ama utakutana na nani, Young Africans wana sifa hiyo kwa sasa, binafsi nimeamua kuwa muwazi kwa sababu naamini kwa sasa Tanzania tumedhamiria kufika mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.” amesema Rage
Katika hatua nyingine Ismail Aden Rage ameipa nafasi Azam FC kwa kusema ina kila sababu za kutinga hatua inayofuata kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Azam FC imepangwa kucheza na Al-Akhdar Sports Club ya Libya, ikianzia ugenini Uwanja wa Omar Al-Mukhtar mjini Bayda mwishoni mwa juma hili, na mwishoni mwa juma lijalo itamalizia nyumbani Dar es salaam.