Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba SC Ismail Aden Rage amesema hana wasiwasi na mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika utakaopigwa Jumapili (Oktoba 09) dhidi ya Mabingwa wa Angola Premeiro De Agosto.

Simba SC itacheza ugenini Estádio França Ndalu mjini Luanda-Angola, kisha mchezo wa Mkondo wa Pili utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Jumapili (Oktoba 16).

Rage amesema Simba SC ina nafasi kubwa ya kusonga mbele katika hatua hiyo kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu, na wanafahamu umuhimu wa Michuano hiyo.

“Simba SC ina nafasi kubwa sana ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya CAF Champions League kwa sababu sisi tunapokuwa tunacheza haya mashindano tunakuwa tunafahamu umuhimu wake ndio maana Simba SC kwenye mashindano ya CAF Champions League hatukamatiki” amesema Rage

Kuhusu Kocha Juma Mgunda, Rage ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania ‘FAT’ kwa sasa Shirikisho ‘TFF’ amesema, Kocha huyo mzawa anapaswa kuaminiwa na kupewa kibarua cha kudumu kuiongoza kikosi cha Simba SC.

Amesema Mgunda tangu alipokabidhiwa jukumu la kuwa Kocha Mkuu Simba SC kumekua na mabadiliko makubwa, hivyo ameutaka Uongozi kuhakikisha unamuamini na kumpa jukumu la kuwavusha na kuachana na Makocha wa Kigeni.

“Kama nikipewa nafasi ya kushauri ningeushauri Uongozi wa timu yangu ya Simba SC imuamini Juma Mgunda na kuendelea nae Kama Kocha Mkuu huenda akatupa kitu cha tofauti na kuishangaza Afrika” amesema

Mgunda alikabidhiwa jukumu la kuwa Kocha Mkuu wa muda Simba SC, baada ya Kocha kutoka Serbia Zoran Maki kuvunjiwa mkataba kwa makubaliano maalum.

Waziri Mchengerwa atembelea klabu ya Fenerbahche-Uturuki
Jeshi la Azam FC kuanza safari ya kuivamia Libya