Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC Ismail Aden Rage amesema hana shaka na kikosi cha klabu hiyo kuelekea mchezo wa kesho Jumapili (Februari 27) wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya RS Berakane.
Simba SC tayari imeshawasili mjini Berkane-Morocco, kwa ajili ya mchezo huo ambao umepangwa kuanza saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki, huku ikiongoza msimamo wa ‘Kundi D’ kwa kumiliki alama 04.
Rage amesema umahiri na utayari wa wachezaji wa Simba SC unamuaminisha utakua kichocheo kikubwa cha kupambania alama tatu kwenye mchezo huo, huku akikumbusha namna walivyoanza kwa kuichapa ASEC Mimosas ya Ivory Coast na kuambulia sare ugenini dhidi ya USGN.
“Sina shaka na kikosi changu cha Simba SC, nina imani kubwa tunakwenda kushinda mchezo wetu na wale warabu, tumeshaonesha sisi ni klabu ya aina gani katika bara la Afrika na kila mtu kwa sasa anatutambua.”
“Tazama tulivyoanza hii michuano tukiwa hapa Tanzania, kulichapa timu kama ASEC Mimosas, sio mchezo, tukaenda ugenini kule Niger tukatoa sare ambayo wengi walikua hawaamini kama matokeo yangekua vile, kwa hiyo nina imani kubwa Simba SC itaendelea kuishangaza Afrika.”
Wakati Simba SC ikicheza ugenini dhidi ya RS Berkane kesho Jumapili (Februari 27), mchezo mwingine wa ‘Kundi D’ utashuhudia USGN ikiendelea kuwa nyumbani mjini Niaemy-Niger kwa kuikaribisha ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ ikiwa na alama 04, ikifuatiwa na ASEC Mimosas yenye alama 03 sawa na RS Berkane, huku USGN ikiburuza mkia wa kundi hilo kwa kumiliki alama moja.