Israel imetangaza kuahirisha mpango wake wa kuwafukuza wahamiaji wa kiume kutoka Afrika na badala yake itawagawa kwenye nchi za Magharibi.
Hatua hiyo ni sehemu ya makubaliano ya Israel na Umoja wa Mataifa. Nchi zilizotajwa kupata gawio la wahamiaji hao ambao jumla yao ni 16,250 ni pamoja na Canada, Italia na Ujerumani.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema kuwa idadi kama hiyo itabaki nchini humo na kupewa makazi.
Hata hivyo, tamko hilo la Netanyahu limepingwa na Italia kupitia kwa waziri wake wa mambo ya nje kuwa nchi hiyo sio sehemu ya makubaliano hayo.
Mpango wa kwanza wa Israel kuwapeleka wahamiaji hao kwenye nchi za Afrika zikiwemo Uganda na Rwanda, ulipingwa vikali na wanaharakati nchini Israel na kuibua maandamano.
Mahakama ya Juu ya Israel iliweka zuio la mpango huo wa kuwasafirisha wahamiaji hao, mpango uliatakiwa kuanza kutekelezwa leo (Jumapili).