Hali imezidi kuwa tete Mashariki ya kati mara baada ya Rais wa Palestinian, Mahmoud Abbas kukata mawasiliano na Serikali ya Israel hivyo kuzidisha mzozo ambao umekuwa ukitokota wiki nzima kuhusu hatua kali zaidi zinazochukuliwa na Israel huko mji wa kale wa Jerusalem.
Hatua hiyo imekuja mara baada ya Wapalestina watatu kuuwawa katika mapigano makali yaliyoibuka dhidi ya polisi wa Israel katika eneo hilo ambalo limekuwa likigombewa na pande zote mbili.
Aidha, mzozo huo ulizuka mara baada ya polisi wa Israeli kuweka vizuizi kuwa wanaume wote chini ya umri wa miaka 50 kushiriki salah ya Ijumaa katika msikiti wa Al-Aqsa eneo linalogombaniwa na pande hizo mbili kinzani.
Hata hivyo, eneo hilo linalogombaniwa ni eneo takatifu la ibada mjini Jerusalem, maarufu kama Hara al-Sharif, kwa waumini wa kislamu na Hekalu la mlimani kwa wayahudi, lakini taarifa zingine zimesema kuwa katika mzozo huo pia Waisrael watatu waliuawa katika eneo la ukingo wa Magharibi la West Bank.