Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameionya Iran kutoingilia anga yake na kujaribu kuweka makazi ya kudumu ya kijeshi kwenye ardhi na anga ya Syria.
Akionesha kile alichodai ni kipande cha mabaki ya ndege isiyo na rubani ya Iran kwenye mkutano wa usalama uliofanyika jijini Munich, Netanyahu alieleza wazi kuwa waliitungua ndege hiyo baada ya kuingia kwenye anga yake.
“Msiijaribu Israel. Hiki ni kipande cha ndege ya Iran isiyo na rubani (drone), au masalia baada ya sisi kuitungua,” alisema Netanyahu.
Alisema kuwa waliitungua ndege hiyo Februari 10 mwaka huu baada ya kuingia kwenye anga yake ikitokea nchini Syria.
Waziri Mkuu huyo pia alidai kuwa baada ya kukifanyia uchunguzi kipande hicho cha ndege walibaini kina mfanano mkubwa na ndege isiyo ya rubani ya Marekani ambayo ilitunguliwa na kushikiliwa na Iran mwaka 2011.
Alimtaja Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Zarif akimkejeli kwa kumuita ‘mdomo wa maneno laini wa utawala wa Iran’ akidai kuwa anafahamu ataikana ndege hiyo iliyotunguliwa.
- Video: Diamond akionesha vifaa vya gharama vya Wasafi radio na Wasafi TV
- Wolper: Tanzania jina la nchi yetu naona si tamu tena na limeanza kuwa chungu
Taharuki kubwa imeibuka kati ya nchi hizo hususan katika miezi ya hivi karibuni baada ya Israel kuhofia kuwa Iran inataka kuanzisha uwepo wa kudumu nchini Syria.
Hatua hiyo inatafsiriwa kuwa tishio kwa Israel ambayo iko karibu na Syria huku ikiwa na uhasama mkubwa na Iran.