Jeshi la Israel limedai kuwa limeitungua ndege ya kivita ya Syria ambayo ni mshirika mkuu wa Urusi, katika vita inayoendelea ndani ya ardhi ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la Israel, Lieutenant-Colonel Jonathan Conricus, ndege hiyo ya kivita aina ya Sukhoi fighter ilipigwa baada ya kuingia kwenye anga la Israel la Golan na kuangikia maeneo ya kusini mwa Syria.
Msemaji huyo wa Jeshi alisema kuwa ndege hiyo ilikuwa inaingia Israel kwa kasi lakini baada ya kugusa anga hilo kwa umbali wa Kilometa 2 walifanikiwa kuiangusha. Lakini hakueleza wazi idadi ya waliopoteza maisha kwenye ndege hiyo.
Hata hivyo, Serikali ya Syria imekanusha vikali kuingilia anga la Israel. Kupitia taarifa yake imesema kuwa adui wake wameitungua ndege ya kivita iliyokuwa inapambana na kundi la kigaidi la Islamic State of Iraq and the Levant (ISIL), Kusini mwa Syria.
“Jeshi la Israel limethibitisha kuunga mkono makundi ya kigaidi na limeidungua moja kati ya ndege zetu za kivita, ambayo ilikuwa inalenga makundi ya kigaidi katika eneo la Saida, eneo lililoko ndani ya anga la Syria,” taarifa ya Serikali ya Syria imesomwa kupitia kituo cha habari cha SANA.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Israel imechukua hatua hiyo baada ya kuona kuwa jeshi la Syria limefanikiwa kuwathibiti waasi na magaidi katika eneo hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2011.
Syria inaungwa mkono na Urusi katika vita hiyo huku Israel na Marekani ikiwapa nguvu waasi dhidi ya Serikali ya Rais Al Assad.