Wakati Kocha Mkuu wa timu za taifa za vijana, Kim Poulsen akitarajiwa kutangaza kikosi cha vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 – Ngorongoro Heroes, nyota wa timu hiyo Issa Abdi Makamba anaendelea vema na matibabu jijini Dar es Salaam.

Kim Poulsen atazungumza na wanahabari kesho Ijumaa saa 5.00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Hosteli za TFF, kuzungumzia kwa kina timu hiyo na kambi ya vijana 50 ambao atawaita kesho.

“Vijana nitakaowataja kesho, wataingia kambini kwa wiki tatu. Muda wa siku 20 mpaka 21 unatosha kabisa kufanya mchujo wa kupata wachezaji 30 ambao wataunda kikosi kipya cha Ngorongoro Heroes,” amesema Kim.

Kocha huyo raia wa Denmark alisema: “Hata nahodha wa Serengeti Boys ana nafasi. Najua anaendelea na matibabu, lakini atakuwepo kwa sababu vijana wale wote waliounda Serengeti Boys watapewa nafasi,” amesema.

Serengeti Boys ni timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ambayo Mei, mwaka huu ilishiriki fainali za AFCON huko Gabon ambako Makamba aliumia kabla ya kuanza kucheza.

Akizungumzia kuhusu afya ya Makamba ambaye aliumia kidole cha mwisho katika mguu wake wa kushoto, Daktari wa timu hiyo, Shecky Mngazija, amesema: “Makamba anaendelea vema mwezi wa 10 anaweza kuanza mazoezi.”

Mchezaji huyo yuko Dar es Salaam kwa takribani mwezi mmoja, akiishi hotelini ambako malazi na chakula – vyote kwa pamoja yanalipwa na TFF sambamba na matibabu yake.

Matibabu ya Makamba yanasimamiwa na Dkt. Paul Marealle ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya TFF na Mjumbe wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).

Amuua mwenzake kisa mabishano kuhusu makalio ya mwanamke
Kuziona Tanzanite, Falconets Tsh. 500, 1000