‘Leo ni leo’, utakaposhuhudiwa mtanange mkubwa zaidi kwenye maisha ya soka duniani kwa mwaka 2018, pale Croatia itakapominyana na Ufaransa kuwa bingwa wa Kombe la Dunia mwaka huu kutokea uwanja wa Luzhniki jijini Moscow, nchini Urusi.
Ingawa Ufaransa ni kisu kikali kinachokata kote, ni kosa la karne kuwachukulia poa Croatia ambao wameshaonesha maajabu katika njia finyu walizopitia kwa kasi.
Tunaitaja zaidi Croatia kwani wao ni mara yao ya kwanza kufikia katika hatua hii kwenye historia ya Fainali za Kombe la Dunia, ingawa awali iliwahi kushiriki mara nne (1998, 2002, 2006 na 2014). Ilizaliwa baada ya kujitenga na Yugoslavia mwaka 1991.
Tofauti na wepinzani wao Ufaransa ambao wamewahi kushinda kombe hilo mara moja huku ikiwa mara yao ya tatu kucheza fainali, kati ya mara sita ilizowahi kushiriki.
Hivyo, endapo Croatia itashinda leo, itaweka historia ya kushinda kombe hilo kwa mara ya kwanza.
Pia, kocha wa kikosi hicho, Zlatko Dalic atakuwa ameweka historia ya mafanikio akikinoa kikosi hicho kwa muda mfupi, miezi tisa tu akichukua kijiti kutoka kwa mtangulizi wake. Dalic alianza kukinoa kikosi hicho Oktoba 7, 2017, baada ya Shirikisho la Soka la Croatia kumtimua Ante Cacic.
Kocha Dalic atakoreza wino wa rekodi itakayobaki kwenye historia ya vitabu vya soka, kwa uamuzi wake wa kumrejesha nyumbani mshambuaji nyota na tegemezi, Nikola Kalinić wakati timu hiyo ikiingia kwenye mzunguko wa 16 bora, baada ya mchezaji huyo kuonesha ukaidi na visingizio akikataa kucheza dakika za mwisho za mechi dhidi ya Nigeria.
Hivyo, itakuwa Dalic amechukua uamuzi kama meneja na kufanikisha bila Nikola Kalinić, ingawa hata akiishia nafasi ya pili sifa hiyo itabaki. Nikola Kalinić anatajwa kugoma kwa visingizio vilevile wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Brazil na pia katika nyakati tofauti mazoezini.
Kadhalika, Croatia itaweka historia ya kuwa timu ya pili kushinda kombe la dunia ikiwa na idadi ndogo zaidi ya watu (Milioni 4.17). Idadi hiyo inakaribiana na wakaazi wa Jiji la Dar es Salaam, ambao ni Milioni 4.4 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Nchi itakayoendelea kuwa na historia ya kushinda kombe la dunia ikiwa na idadi ndogo zaidi ya watu ni Uruguay ambayo ilishinda kombe hilo ikiwa na watu takribani milioni 1.7 tu.
Lakini kwa upande wa Ufaransa, ushindi wa leo utaikata kiu ya miaka 20 ya kusubiri kutwaa tena kombe hili, tangu ilipoivuruga Brazil 3-0 mwaka 1998, Ufaransa wakiwa wenyeji.
Hii ni fainali ya tatu kwa Ufaransa, mwaka 1998, 2006 na leo.
Kylian Mbappé anapewa nafasi zaidi ya kung’ara kwenye mashindano haya, kwa kuzingatia kuwa wale mafahari watatu Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Neymar Jr. walishatupwa nje ya mashindano.