Mshambulizi wa Brentford ya Ligi Kuu England Ivan Toney ameshtakiwa na Chama cha Soka England ‘FA’ kwa kukiuka sheria zao za michezo ya kubashiri kwa zaidi ya mara 232.
Toney mwenye umri wa miaka 26 ambaye hakujumuishwa kwenye Kikosi cha wachezaji 26 cha England kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia, alifichua kwamba amekuwa akiisaidia FA katika maswali yake kutokana na madai kwamba alicheza kamari kwenye mechi.
“Nimekuwa nikisaidia Chama cha Soka kwa maswali yao lakini sitatoa maoni yoyote hadi uchunguzi huo utakapokamilika.”
“Najivunia kama raia wa England na imekuwa ndoto yangu ya utotoni kuichezea nchi yangu katika fainali za Kombe la Dunia.” amesema
Hizi ni tuhuma nzito dhidi ya Toney, na amepewa muda majuma mawili kukata rufaa dhidi ya mashtaka yanayomkabili.
Kufuatia habari hii klabu yake ya Brentford imetoa taarifa ikisema inaendelea na mazungumzo na Toney na wawakilishi wake kuhusu suala hilo, lakini hawatatoa maoni zaidi kwa sasa.
Mashabiki wa Brentford wanatumai kuwa repoti hizi hazitakuwa na athari mbaya kwa nyota huyo kwani kiwango chake kimekuwa chachu ya mafanikio ya klabu hiyo hadi mapumziko ya fainali za kombe la Dunia 2022.