Mbunge wa Nzega Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Bashe amesema kuwa kitendo cha makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana kumuandikia barua katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho wakilalamika kudhalilishwa, ni mkakati unaolenga kumkosesha uhalali Rais John Magufuli kuwania urais 2020.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa tamko la makatibu wakuu hao wastaafu walilomuandikia katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu, Pius Msekwa, limekwenda kinyume cha Katiba ya CCM.
“Wao wenyewe wamesema kuwa hawamtafuti Musiba bali anayetoa kinga, sasa mimi sipendi kumung’uunya wala kuzunguka mambo hapa wanamlenga Rais Magufuli, hatuwezi kuruhusu Magufuli ni mwenyekiti wetu, ni mgombea wetu wa urais 2020, ‘iwe jua au mvua’ hatuwezi kuruhusu hatua ambayo inadhoofisha uhai wa chama,”amesema Bashe.
Aidha, Nape amekitaja kifungu 122 (1) cha Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, akisema kuwa kimekiukwa na tamko hilo kwa kuwa baraza hilo halina mamlaka ya kusikiliza malalamiko hayo.
“Ukiwa na malalamiko lazima ujue wa kumwandikia. Mimi nikilalamikia gazeti namwandikia editor (mhariri) ndio ana mamlaka ya kisheria, siwezi kumwambia circulation manager (meneja usambazaji),” ameongeza Bashe.
Amebainisha kuwa kosa jingine lililofanywa na makatibu hao kwenye waraka wao ni kuuweka hadharani, ambapo amesema kuwa wanajua vizuri Katiba, miiko na tamaduni za Chama chao, na kwamba unapeleka malalamiko ya mwanachama kwenye chama, Musiba si mwanachama wa CCM.
Hata hivyo, ameongeza kuwa linapokuja suala la CCM ni lazima waungane na kusema kuwa Mzee Msekwa anaelewa kilichofanywa na akina Kinana ni kinyume na Katiba na ndio maana amesema suala hilo amepeleka kwenye chama
Bashe amemalizia kwa kusema kuwa “Bila kujali kama ni Mbunge au sio Mbunge kama ni MwanaCCM hatuwezi kuruhusu anachofanya Kinana na ile timu. Na ninaweza kuapa kuwa Makamba hana Maandishi yake mule.