Uongozi wa klabu ya Chelsea unatarajiwa kutuma ofa ya usajili wa mlinda mlango kutoka nchini England na klabu ya Stoke City Jack Butland, ili kumaliza sintofahamu iliyozuka katika lango lao, kuelekea msimu mpya wa ligi.
Chelsea wanajipanga kufanya hivyo kabla ya siku ya Alhamis ambayo itakua mwisho kwa usajili wa majira ya kiangazi nchini England, kutokana na mustakabali wa mlinda lango wao kutoka nchini Ubelgiji Thibaut Courtois kuwa shakani.
Courtois amekua katika shinikizo la kutaka kuondoka klabuni hapo na kujiunga na mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, baada ya kukataa kusiani mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia The Blues.
Uongozi wa Chelsea kwa kushirikiana na benchi la ufundi unaamini mlinda mlango Butland atakua chaguo sahihi, ambalo litaweza kuziba pengo la Courtois kama atakamilisha mipango yake ya kuihama klabu hiyo.
Tayari mazungumzo ya awali baina ya viongozi wa klabu za Chelsea na Stoke City yameshaanza kwa njia ya simu, na wakati wowote kuanzia leo huenda ofa ya usajili wa Butland ikawasilisha huko Stoke On Trent.
Thamani ya usajili wa mlinda mlango huyo ambaye huenda akarejea ligi kuu msimu wa 2018/19 inatajwa kuwa Pauni milioni 30.
Butland alikua sehemu ya kikosi cha Stoke City kilichoshuka daraja mwishoni mwa msimu uliopita, na tayari ameshaitumikia klabu hiyo katika mchezo wa ufunguzi wa ligi daraja la kwanza msimu huu mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Leeds Utd waliochomoza na ushindi wa mabao matatu kwa moja.