Manchester City imetamba kuwa itakuwa ngumu kuzuilika nyumbani katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Nusu Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Real Madrid, amesema winga Mabingwa hao wa England, Jack Grealish.
Manchester City ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Madrid katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza uluofanyika kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu jijini Madrid juzi Jumanne (Mei 09) na kuifanya City kuwa katika nafasi nzuri ya kutinga Fainali.
Man City ilipata sare hiyo baada ya mchezaji wake, Kevin De Bruyne kusawazisha kufuatia bao la kuongoza lililofungwa na Vinicius Jr, ambalo liliifanya Real Madrid kuwa mbele.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya hawajafungwa nyumbani tangu Novemba mwaka jana na wanatarajia kuendeleza rekodi yao Mei 17, wakati timu hizo zitakaporudiana.
“Kwenye Uwanja wa Etihad, kwa kweli tunahisi hakuna timu inaweza kutuzuia kupata ushindi,” amesema Grealish.
“Tulikuja hapa (kwenye Uwanja wa Bernabeu) kujaribu kupata ushindi, lakini tumeonesha uwezo wetu kwani tulikuwa nyuma lakini tukasawazisha.
“Mwishoni nafikiri yalikuwa matokeo sahihi. Walikuwa na nafasi zao na sisi tulikuwa nazo chache.”
Man City inasaka mataji matatu, tayari imekata tiketi ya kucheza fainali ya mashindano ya Kombe la FA na wanaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya England kwa tofaui ya pointi moja huku wakiwa na mchezo mkononi zikiwa zimebaki mechi nne.
Grealish amesema timu yake wamejifunza mengi tangu walipotolewa na Real Madrid katika mchezo wa Nusu Fainali wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya msimu uliopita.
“Mwaka huu tuna kikosi kipya, wachezaji tofauti. Tuna muungano imara wa wachezaji wenye uzoefu duniani na wale vijana,” aliongeza kiungo huyo wa kimataifa wa Uingereza.”
Mlinda Lango wa Real Madrid, Thibaut Courtois amesema mchezo wa marudiano utakuwa kama fainali kwa timu hiyo ya Hispania, ambayo ina rekodi ya kutwaa taji hilo mara 14 ikiwa bingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Wiki ijayo itakuwa kama fainali,” alisema Courtois “Natumaini tunaweza kufanya vizuri, tutakuwa nyumbani kwa City na itakuwa ngumu kwetu.”