Uongozi wa mabingwa wa kombe la shirikisho (ASFC) Azam FC unatarajiwa kumtangaza mkuu mpya wa kitengo cha habari na mawasilino, wakati wanajiandaa kuelekea mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya mabingwa tetezi Wekundu Wa Msimbazi Simba.
Mpango wa kubadilishwa kwa mkuu wa kitengo hicho, umefahamika kufuatia aliyekua akihudumu nafasi hiyo Jaffar Iddy Maganga kutuma taarifa katika vyombo vya habari akithibitisha kuhamishwa kitengo.
“leo, Machi 2, 2020 rasmi sitakuwa Afisa Habari wa Azam FC, kampuni imenibadilishia majukumu na nitaendelea kuwa mwanafamilia wa Azam FC, naomba ushirikiano uendelee kuwepo kati ya huyo ambaye atakuja kwani sote ni ndugu,” amesema.
“Mimi sitakuwepo katika nafasi hii lakini nitaendelea kuhudumu ndani ya Azam, ninaomba yule atakayekuja mumpe ushirikiano. Kama nimewakosea mnisamehe na yule atakayekuja kama mtaona anakwenda tofauti mwambieni ile aende sawa nanyi”, ameongeza.
Jaffar Iddy Maganga anaondoka kwenye nafasi hiyo baada ya kuhudumu nafasi ya mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa Azam FC kwa zaidi ya miaka kumi.
Azam FC itakuwa mwenyeji wa Simba katika mchezo wa ligi utakaopigwa Machi 4 katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, Simba ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 65 huku Azam FC ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi 48.