Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika Namungo FC wameendelea na mkakati wake wa kukitengeneza kikosi chao kwa kumsajili aliyekuwa beki wa kushoto wa Young Africans, Jaffar Mohamed Mbena.
Jaffar, ametambulishwa kwenye mtandao rasmi wa klabu hiyo ambao pia umeeleza viongozi wa klabu hiyo wanafuraha kukamilisha usajili wa beki huyo kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Jaffar anakuwa ni mchezaji wa tano kusajiliwa na Namungo FC yenye maskani yake Ruangwa mkoani Lindi, katika kipindi hiki cha dirisha la usajili kuelekea msimu wa 2020/21.
Wengine waliosajiliwa klabuni hapo ni Abdulhalim Humud kutoka Mtibwa Sugar, Steven Sey, Mghana aliyekuwa akiichezea Singida United, Fred Tangalo kutoka Lipuli na Sixtus Sabilo akisajiliwa kutoka Polisi Tanzania.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Zidadu amesema wanatarajia kuingia mkataba na Kocha Mkuu, Hitimana Thiery baada ya kurejea nchini akitokea kwao alikokwenda kwenye msiba wa mdogo wake.
“Tulikuwa tuingie naye mkataba, lakini haikuwezekana kwa sababu alipata msiba, isingewezekana akae na sisi kuzungumzia masuala ya mkataba wakati amefiwa, hivyo tukaona kwanza aende akahudhurie mazishi kwanza, halafu akirudi atakuwa ametulia, lakini kila kitu kiko vizuri,” alisema Zidadu.