Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amesema watumiaji wote waliopo kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji, wanapaswa kuheshimu sheria ya mazingira.
Jafo ameyasema hayo wakati ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wadau, wawekezaji wa Bonde la Usangu, wakulima wa mpunga, wamiliki wa mashine za kukoboa mpunga na wafugaji Januari 16, 2023 Mkoani Mbeya.
Amesema, “Watumiaji wote waliopo kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji, wanapaswa kuheshimu sheria ya mazingira, Serikali haitawanyamazia wale wote ambao wataharibu au kuvunja sheria hizo.”
Akiwa Mkoani Mbeya, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kuitoa nje ya hifadhi ranchi ya Usangu kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa kisasa ambapo pia mgogoro wa matumizi ya ardhi Wilayani Mbarali mkoani Mbeya uliodumu kwa miaka 15, uliokuwa ukihusisha wakazi wa Wilaya hiyo katika eneo la Bonde la Usangu dhidi ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ulimalizwa.