Halmashauri nchini zimetakiwa kufungua akaunti maalumu zitakazowekwa asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya makundi mbalimbali ya wanawake, vijana na watu wenye ulamavu ifikapo Novemba 30, 2019.

Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati akifunga kongamano la wataalamu wa maendeleo ya jamii.

Amesema agizo hilo si geni kwakua lilishawahi kutolewa hapo awali lakini halmashauri nyingi hazikutekeleza na kulazimika kurudia kuagiza tena hadi ifikapo Novemba 30, 2019 halmashauri zote 185 nchini ziwe zimekamilisha zoezi hilo.

“Niliwahi kutoa agizo la kutaka halmashauri kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya fedha za mikopo kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu sasa kwa mara ya mwisho ikifika Novemba 30 mwaka huu, halmashauri zote zihakikishe zimefungua akaunti maalumu,” amesema Waziri Jafo.

Amesema kitendo cha kuweka fedha hizo kwenye akaunti moja kinachangia kutotambua kwa ufasaha matumizi na ufuatiliaje wake hivyo ni vyema Halmashauri zikatenga akaunti hizo ili kufanikisha malengo kusudiwa.

Aidha Jafo ameahidi kuangalia namna wizara yake itakavyofanikisha kutenga fedha kwa ajili ya wataalamu wa maendeleo ya jamii ambazo watazitumia kwenye ufuatiliaji na tathimini ya fedha zilitolewa katika makundi mbalimbali.

“Kutokuwa na uwezeshaji huo itakuwa ni vigumu kwa maafisa maendeleo ya jamii kufuatilia uendelevu wa vikundi vilivyokopa kwani fedha hizo zinatolewa ili kuweza kubadilisha maisha ya wananchi,” amesema Jafo.

Awali Katibu Mkuu Wizara ya afya Maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Idara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema anaamini baada ya mkutano huo maafisa maendeleo watafanyia kazi yale yote waliyoyapata ili kuleta mabadiliko ya kimaendeleo.

Hamisa Mobetto avuka mipaka kwa mama yake mzazi
Video: RC Makonda awasweka rumande wakandarasi kampuni za kichina