Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amewaasa wachimbaji wadogo wa dhahabu kutumia teknolojia mbadala wa miti katika shughuli zao.
Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam na kusema uchumi unaotokana na uchimbaji wa madini ni muhimu lakini wachimbaji katika maeneo mbalimbali nchini wanapaswa kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
Amesema, “kumekuwa na uharibifu wa mazingira katika maeneo ambayo shughuli hizo zinafanyika ambapo wachimbaji wadogo wanakata miti kwa ajili ya kujengea mashimo hivyo ni wakati sasa kwa wachimbaji hao kuanza kutumia chuma.”
Akizungumzia suala la uchimbaji wa mchanga hususan katika mkoa wa Dar es Salaam, amesema jambo hilo lina changamoto kutokana na wachimbaji kufanya shughuli bila kufuata utaratibu hali inayosababisha uharibifu wa mazingira.
“Ni kweli tuna changamoto kubwa ya uchimbaji wa madini ya mchanga na watu wanaacha makorongo baada ya kuchimba kwa mfano kule Kigamboni wanaharibu mazingira, wapo baadhi ya watu tunashukuru wanafukia mashimo baada ya uchimbaji,” amesema Jafo.
Hata hivyo, Dkt. Jafo amefafanua kuwa shughuli yoyote ya uchimbaji lazima ipate kibali cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).