Wakurugenzi 10 walioteuliwa hivi Karibuni na Rais John Pombe Magufuli, wametakiwa kujiamini na kusimamia majukumu yao kikamilifu ikiwemo kuyalinda mahusiano mema ya Utumishi.

Wito huo umetolewa hii leo jijini Dodoma na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo, wakati akifungua kikao kazi kilichoambatana na kiapo cha utumishi kwa Wakurugenzi hao.

Amesema suala la kusimamia majukumu, mahusiano mema na Maadili ni jambo la msingi kwa kila mtumishi wa Serikali, na kuwataka kutokuwa chanzo cha migogoro katika Halmashauri walizopangiwa.

“Simamieni vyema majukumu yenu na pia msisahau suala la mapato na ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, maana  msipozingatia mambo haya halmashauri zenu zitayumba kwa kukosa mapato,” amesema Jafo.

Naye Kaimu katibu Mkuu TAMISEMI, Mathias Kabundugulu amewataka wakurugenzi hao kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kusimamia vyema uchaguzi wa serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika nchini kote Novemba 24 mwaka huu.

Uteuzi wa Viongozi hao ulifanywa na Rais John Pombe Magufuli Oktoba mosi mwaka huu, kwa kuwateua Wakurugenzi watendaji wapya wapatao kumi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa, na kuwahamisha vituo vya kazi wengine wawili.

Dkt. Abbasi: Tanzania imeongoza kupunguza umasikini, TRA imevunja rekodi
Video: Wananchi wafunguka kuhusu Serikali za mitaa