Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amewataka wananchi kulinda miradi ya maendeleo, hifadhi ya mazingira kwa kupanda miti pamoja na kulinda uoto wa asili ili iendelee kudumu.
Jafo ametoa rai hiyo leo hii leo Mei 3, 2023 wakati akizindua miradi mbalimbali kupitia Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mingo wakati wa ziara ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia
Vijijini (EBARR) unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Mei 03, 2023 ambapo ametoa wito kwa wananchi kuitunza miradi hiyo.
Amesema, miradi hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 520 ikiwemo uchimbaji wa visima viwili virefu vya maji inajumuisha mfumo wa sola kwa ajili ya kuvuta maji, matanki ya kuhifadhi maji pamoja na mfumo wa umwagiliaji na wa matumizi ya wananchi, lambo la lenye uwezo wa kukusanya maji lita za ujazo 252,299 zikiweza kumwagilia hekta 287 za mazao ya mbogamboga, kiwanda kidogo cha sabuni na kikundi cha uzalishaji uyoga.
Aidha ameongeza kuwa, Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha wananchi katika maeneo yenye ukame wanapata mafaniki na inapeleka miradi kwa wananchi ili kuwasaidia katika kupata fursa za kimaendeleo pamoja licha ya kuwepo kwa changamoto za mabadiliko ya tabiachi zinazochangia ukame.
Dkt. Selemani Jafo akikagua kitalu nyumba ambacho kimejengwa sambamba na kisima cha maji kinachojumuisha mfumo wa sola kwa ajili ya kuvuta maji wakati wa ziara yake ya kuzindua Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi . Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli.
“Ndugu zangu niwashukuru sana kwa kutekeleza hii miradi na niwaombe tuilinde asitokee mharibifu akaja kuharibu miundombinu tumsimfumbie macho, lakini pia ajenda yetu kuu tutunze mazingira, usipoyatunza na kuyashughulikia mazingira yatakushughulikia”, amesisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli amemshukuru Waziri Jafo kwa kutembelea wilaya hiyo na kuzindua miradi hiyo kwa manufaa ya wananchi na kuahidi kushirikiana na timu yake kuisimamia na kuilinda miradi hiyo ya maendeleo kwa nguvu zote kuhakikisha inakwenda kwa wananchi kama ambavyo Serikali inaagiza.