Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amewataka wanaume ambao hawajafanyiwa tohara katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara nchini kuhakikisha wanajitokeza kufanyiwa Tohara ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini.
Akizindua magari kwa ajili ya utoaji wa huduma tembezi za Tohara (Maounted mobile Clinic Vans) kwa wanaume leo katika Ofisi za Rais –TAMISEMI, mtumba jijini Dodoma Waziri Jafo amesema kuwa kuna faida kubwa kwa wanaume kufanyiwa tohara.
“Wale ambao hawajapata Tohara, waende wakapate tohara kwa kuwa uwekezaji huu mkubwa umekuja kwenu, kupata huduma tembezi za tohara, ni fursa ya kipekee sana, haijawahi kutokea katika maeneo mengine, tumieni fursa hiyo,” amesema Jafo.
Jafo amefafanua kuwa ipo mikoa 16 ambayo ina changamoto kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kutokana na watu kukosa kufanyiwa tohara, hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kujikinga na maambukizi ya UKIMWI nchini.
Amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa za wataalam, wale ambao wamepata tohara wana asilimia kubwa ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa asilimia 60.
“Tohara inasaidia kupunguza magonjwa ya kuambukiza yanayoendana na ngono kama kaswende lakini pia inaonekana wazi kwamba waliofanyiwa tohara wanapata nafuu nyingi sana katika suala la afya na mazingira yao,” amefafanua Waziri Jafo.
Aidha, amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri katika Mikoa iliyopatiwa magari kufanya uratibu mzuri kwa kupanga vizuri jinsi magari hayo yatakavyofanya kazi na kuwasaidia wananchi na kuwataka kuhakikisha wanalinda na kutunzwa kwa magari na vifaa vyake.
Wakati huohuo, Mkurugenzi Mkazi Interhealth International Dkt. Lucy Raymond amesema wanaume zaidi ya 1,820,000 wamepatiwa huduma ya tohara na watumishi 1,000 wa afya wamepatiwa mafunzo ya utoaji huduma bora za tohara, usimamizi wa ubora na uhifadhi wa takwimu tokea mwaka 2010 hadi sasa.